Lemah: Tuzo hii ni chachu kuendelea kumtumikia Mungu

BAGAMOYO: Mshindi wa tuzo ya Muimbaji bora wa Kiume katika tuzo za TASUBA Awards 2026, Erick Lemah amesema hatua hiyo ni neema ya Mungu na chachu ya kuendelea kumtumikia kupitia muziki wa Injili.
Akizungumza na Spoti Leo, Erick amesema anajivunia ushindi huo huku akimpa Mungu utukufu kwa mafanikio aliyoyapata.
“Kwa unyenyekevu mkubwa namshukuru Mungu kwa neema hii. Ushindi huu si wangu peke yangu, ni wa kila mmoja aliyeniunga mkono kwa kura, maombi, upendo na kuendelea kuamini muziki wangu,” amesema Erick.
Ameongeza kuwa anawashukuru familia yake, mashabiki, marafiki na waandaaji wa TASUBA Awards kwa mchango wao katika kufanikisha ushindi huo.
“Kila kura yenu imeandika historia. Tuzo hii inanipa nguvu ya kuendelea kutengeneza muziki wenye kugusa maisha ya watu na kumtukuza Mungu. Huu ni mwanzo wa mambo makubwa zaidi,” amesema.
Erick amewashukuru wote waliompigia kura na kusisitiza kuwa ushindi huo ni wa kila mmoja aliyekuwa sehemu ya safari yake ya muziki.
“Asanteni sana kwa kunichagua kuwa Muimbaji Bora wa Kiume wa TASUBA Awards 2026. Ushindi huu ni wa wote waliosimama nami. Mungu awabariki,” amesema.




