Muziki

Diamond: Zamu yetu itafika kimataifa

MSANII wa muziki wa kizazi kipya Nassibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amesema ujio wa Tuzo za Kimataifa za Trace hapa nchini ni upendeleo. Aidha, amesema licha ya muziki wa Afrika Mashariki kutong’ara kimataifa siku moja zamu yao itafika.

Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika Zanzibar Februari 26 mwaka huu ambapo inategemewa kuwaleta wasanii wengi wa kimataifa.

Diamond katika mahojiano yake na Redio Hot ya New York Marekani amenukuliwa akisema ujio wa tuzo hizo ni fursa kwa Tanzania kutangaza uzuri wake.

“Kufanyika kwa tuzo hizo nchini ni jukwaa kubwa linalofuatiliwa na mamilioni ya watu duniani. Mbali na kuonesha vipaji tunapata nafasi ya kuonesha uzuri wa nchi,”amesema.
Amezungumzia muziki wa Afrika Mashariki kutotambulika kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika Magharibi na Afrika Kusini akisema muda wake utafika.

“Tukubali kwamba ni zamu kwa zamu, muziki wa Afrika ulianza kufanya vizuri DRC, ikiafuatiwa na Afrika Kusini, Nigeria na imerudi tena kwa Afrika Kusini,”ameongeza.

Nyota huyo amesema anaamini kabisa wanaofuata kufanya vizuri ni Tanzania hasa baada ya mwaka jana kuachia nyimbo mbili za kimataifa za Shuu na Komasava zilizofanya vizuri.

“Uliona wasanii wakubwa kama Chris Brown, Jason Derulo na Travis Scott waliucheza wimbo huu, inaonesha ni jinsi gani tumeanza kukua,”amesema.

Related Articles

Back to top button