EPL

Jeff Bezos kuimiliki Liverpool

LIVERPOOL: Mpango wa uwekezaji wa mfanyabiashara bilionea Jeff Bezos katika klabu ya Liverpool umeibua uwezekano wa mabadiliko makubwa ya umiliki wa klabu hiyo katika kipindi cha miezi 12 ijayo.

Kundi la wawekezaji linalojulikana kama 1892 Holdings, linaloongozwa na Amit Bhatia na kumjumuisha mwanzilishi wa Amazon, Jeff Bezos, limepata haki ya kwanza ya kununua hisa za udhibiti wa Liverpool, iwapo wamiliki wa sasa, Fenway Sports Group (FSG), wataamua kuuza au kupunguza umiliki wao katika kipindi hicho.

Hata hivyo, hatua hiyo haimaanishi kwamba Liverpool inauzwa kwa Bezos kwa sasa.
FSG bado inamiliki hisa nyingi za Liverpool na inaendelea kuwa na udhibiti wa uendeshaji wa klabu hiyo. Taarifa za sasa zinaeleza kuwa FSG haijaweka ahadi rasmi ya kuuza hisa zake zinazobaki kwa 1892 Holdings.
Kwa mujibu wa The Guardian, 1892 Holdings imenunua takribani asilimia 38 ya Liverpool, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko asilimia 30 iliyokuwa imeripotiwa awali. Thamani ya dili hilo inakadiriwa kuwa zaidi ya pauni bilioni 2, huku ikidaiwa kuwa itaipa Liverpool thamani ya takribani pauni bilioni 5.5.

Ikiwa FSG itaamua kubaki na umiliki wake wa sasa, hakuna kinachobadilika. Lakini endapo itaamua kuuza sehemu kubwa zaidi ya hisa zake ndani ya miezi 12, 1892 Holdings itakuwa katika nafasi ya kwanza kupata hisa hizo na hivyo kuwa mmiliki mwenye udhibiti wa klabu.

Kwa sasa, Jeff Bezos mwenyewe anachukuliwa kuwa mwekezaji asiyehusika moja kwa moja katika uendeshaji wa kila siku wa Liverpool. Anashiriki kupitia K5 Sports, huku mwakilishi wake Bryan Baum akiwa sehemu ya bodi mpya ya klabu.

FSG ilinunua Liverpool mwaka 2010 kwa pauni milioni 300, na hadi sasa imeendelea kuwa mmiliki mkuu wa klabu hiyo.

Related Articles

Back to top button