Ligi Kuu

Ahmed: Dodoma Jiji ni mziki mnene

DODOMA: KLABU ya Simba imesema inatarajia kukumbana na upinzani mkubwa dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kesho.

Imesema mpinzani huyo ana ubora wa juu kuliko waliokutana nao katika mchezo uliopita wa Tanzania Prisons walioibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Akizungumza kuelekea pambano hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kiwango cha Dodoma Jiji FC ni kikubwa na kimekuwa kikiwapa changamoto kila wanapokutana, tofauti na Tanzania Prisons.

“Mechi ya Dodoma Jiji ni bora zaidi na kama unafikiri ushindani tulioupata kutoka kwa Prisons ni mkubwa basi wa Dodoma Jiji utakuwa mkubwa zaidi. Ukiangalia upande wa ubora kati ya Prisons na Dodoma, Dodoma ni bora zaidi,” amesema Ahmed.

Amebainisha kuwa rekodi za michezo ya nyuma zinaonesha ugumu wa timu hiyo kwani Simba imekuwa ikipata ushindi mwembamba mara nyingi, hali inayodhihirisha uimara wa wapinzani wao.

“Sisi wenyewe tumekuwa tukiwafunga Dodoma Jiji kwa tabu sana, mara nyingi ni ushindi wa bao 1-0 kwa misimu kadhaa. Hiyo haiji kwa bahati mbaya, ni kutokana na ubora wa mpinzani,” ameongeza.

Ahmed amesema wanatarajia mazingira magumu zaidi kutokana na Dodoma Jiji kucheza nyumbani kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma huku wakipata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wao.
Pamoja na hilo, amesisitiza kuwa lengo la Simba ni kuondoka na pointi tatu muhimu, akibainisha kuwa wachezaji tayari wamepewa tahadhari kuhusu ubora wa Dodoma Jiji.

Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na dhamira ya kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Related Articles

Back to top button