Ahmed Ally: Simba Tunakwenda Kigoma Kuchukua Pointi Tatu

DAR ES SALAAM: MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema timu hiyo inakwenda Kigoma ikiwa na lengo la kuchukua pointi tatu dhidi ya Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Alhamisi.
Ahmed amesema Simba inautambua ugumu wa mchezo huo kutokana na ubora wa Mashujaa pamoja na benchi lao la ufundi, akimtaja kocha wa timu hiyo kuwa ni mwalimu mzuri mwenye uzoefu wa zamani wa kucheza soka.
“Tunakwenda Kigoma kuchukua pointi tatu. Ni mechi ngumu sana, tunawaheshimu Mashujaa na aina ya mwalimu waliyenaye ni mwalimu mzuri ambaye aliwahi kuwa mchezaji,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa Mashujaa ni moja ya timu ambazo zimekuwa zikiisumbua Simba, lakini safari hii wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi wa kujiamini tofauti na msimu uliopita.
“Tunataka ushindi wa kujiamini, sio ule ushindi wa roho juu juu wa msimu uliopita. Tunafanya mipango yetu ya kiufundi kuhakikisha tunachukua pointi tatu na mnyama anarudi Dar,” amesema.
Ahmed pia amewataka mashabiki wa Simba waliopo Kigoma kujipanga kuhakikisha timu hiyo inakuwa salama na kupata sapoti kubwa katika mchezo huo muhimu.




