MSHAMBULIAJI wa Azam, Prince Dube amesema matarajio yake msimu huu ni kufunga mabao mengi ili kuisaidia timu yake kufikia malengo.
Akizungumza na Spotileo, mshambuliaji huyo amesema matarajiio hayo yanatokana na kuwa fiti msimu huu baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakimsumbua.
“Msimu uliopita sikuwa kwenye kiwango changu kutokana na majeraha ya goti lakini nafurahi msimu huu nimekuwa na mwanzo mzuri hivyo naamini nitatimiza malengo yangu,” amesema Dube.
Kwa mujibu wa mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe mpango wake msimu huu ni kufunga zaidi ya mabao 15.
Tangu kuanza kwa msimu huu Dube ameifungia Azam bao moja pekee katika michezo minne ambayo Azam imecheza.
Azam imeondoka leo kwenda Ndola, Zambia kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo utakaofanyika Septemba 23 katika uwanja wa Levy Mwanawasa.




