
WAKATI kilio kikitanda kwa maafande wa Polisi Tanzania na Ruvu Shooting baada ya kushuka daraja sasa vita ya kubaki ligi kuu Tanzania bara imehamia kwenye maeneo mawili yenye msisimko wa aina yake.
Vita ya kwanza ipo kwenye timu zinazopambana kukwepa kucheza hatua ya mchujo ili kusalia ligi kuu na kwenye mbio za ufungaji bora ambapo Kivumbi ni cha nyota Fiston Mayele wa Yanga mwenye mabao 16 na Saido Ntibazonkiza wa Simba mwenye mabao 15 kila mmoja akiwa amesaliwa na mchezo mmoja.
Timu tano bado hazina uhakika wa kuwepo kwenye ligi kuu Tanzania bara kwa msimu ujao kwani kuna chujio litapita kwa timu zitakazomaliza kwenye nafasi ya 13 na 14 zitakazolazimika kucheza michezo ya mtoano ili kusalia ligi kuu.
Uhakika uliopo ni kwamba kati ya KMC au Mbeya City ni lazima mmoja wao acheze hatua ya mtoano kutokana na timu hzio kukutana zenyewe kwa zenyewe katika mchezo wa mwisho wa ligi kuu utakakaopigwa jijini Mbeya.
Mpaka sasa KMC ipo nafasi ya 14 ikiwa na alama 29 huku Mbeya City ikiwa nafasi ya 13 na alama 31, hivyo hii ni fainali kwa timu hizi mbili.
Timu nyingine ambazo jinamizi hili linawaandama ni Mtibwa Sugar yenye alama 32 kwenye nafasi ya 12 Coastal Union yenye alama 33 nafasi ya 11 na Dodoma Jiji alama 34 kwenye nafasi ya 10 .
Majibu ya ni nani atamezwa kwenye giza la jinamizi hili yatafahamika Juni 9 kwenye michezo ya mwisho ya ligi hiyo.
Ninaacha kitendwawili kwako cha nani atapitiwa na fagio la mchujo.