Tanzania yateuliwa mjumbe CABOS

TANZANIA imeteuliwa kuwa Mjumbe katika Bodi ya Ushauri wa Michezo ya Jumuiya ya Madola(CABOS) kwa kipindi cha 2023/25.

Taarifa ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt Pindi Chana iliyotolewa na wizara hiyo imesema Kaimu Mkurugenzi Maendeleo ya Michezo Ally Mayay Tembele ataiwakilisha Tanzania katika bodi ya CABOS na kuwa mjumbe mwakilishi wa Bara la Afrika.
Hatua hiyo inatokana na kuimarika kwa nyanja ya diplomasia ya nchi ikiwemo ya michezo katika serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
CABOS ni chombo cha kumshauri Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola na serikali wanachama kuhakikisha ushirikishwaji thabiti wa serikali na uwakilishi katika maendeleo ya sera na utekelezaji wake kwa kuzingatia maadili na matarajio ya mkataba wa jumuiya hiyo.