Nyumbani

Mbappe, Lamine Yamal uso kwa uso leo

DALLAS: Nyota wawili wanaotikisa soka duniani kwa sasa, Kylian Mbappe wa Ufaransa na Lamine Yamal wa Hispania, wanatarajiwa kukutana uso kwa uso katika pambano la nusu fainali ya Kombe la Dunia, huku kila mmoja akisaka kuiongoza timu yake kutinga fainali.

Mbappe ameonesha makali makubwa mbele ya lango katika mashindano hayo, akifunga mabao nane kutokana na mashuti 30 aliyopiga, huku pia akitoa asisti tatu na kutengeneza nafasi nyingi zaidi kuliko Yamal.

Kwa upande mwingine, Lamine Yamal amefunga bao moja pekee, lakini ameng’ara kwa uwezo wake wa kupiga chenga, kutengeneza nafasi za wazi na kusaidia timu kujilinda, jambo linalomfanya kuwa silaha muhimu kwa Hispania.

Kocha wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez, aliwahi kumsifu Yamal akisema ana uwezo wa kubadili matokeo ya mechi akiwa na umri mdogo, akimlinganisha na magwiji kama Lionel Messi, Diego Maradona, Pele na Ronaldo Nazario. Xavi pia alieleza kuwa ikiwa ataendelea na kiwango hicho, miaka 15 hadi 20 ijayo inaweza kuwa ya Yamal.

Hii si mara ya kwanza kwa nyota hao kukutana katika mashindano makubwa. Katika nusu fainali ya Euro 2024, Yamal alifunga bao la kusawazisha kabla Hispania haijaibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ufaransa.

Mwaka uliofuata, Hispania iliifunga tena Ufaransa mabao 5-4 kwenye nusu fainali ya UEFA , ambapo Yamal alifunga mabao mawili na Mbappe akafunga moja.

Katika mikutano yao 10 iliyopita, Yamal ameibuka mshindi mara nane, ingawa Mbappe ndiye mwenye mabao mengi zaidi akifunga tisa dhidi ya sita ya Mhispania huyo.

Pambano la safari hii linatajwa kuwa kubwa zaidi katika ushindani wao, kwani mshindi atapata nafasi ya kucheza fainali ya Kombe la Dunia itakayofanyika Julai 19 mjini New Jersey, akiwa na matumaini makubwa ya kunyanyua taji la dunia.

Related Articles

Back to top button