Muziki

Zuchu: Diamond ananipa uhuru na sapoti kwenye kazi

DAR ES SALAAM: MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva, Zuhura Othuman ‘Zuchu’, amesema licha ya kununua gari lake aina ya Bentley kwa uwezo wake, mumewe, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, amekuwa akimpa ushirikiano mkubwa katika shughuli zake za kikazi na maendeleo kwa ujumla.

Akizungumza kuhusu maisha yao ya kimahusiano, Zuchu amesema ni baraka kubwa kwa mwanamke kuwa na mwenzi anayemuunga mkono katika kazi zake na kumpa uhuru wa kufanya mambo yanayomjenga bila vikwazo.

Amesema “katika misingi ya dini yake, mume ana nafasi ya kutoa uamuzi wa mwisho katika baadhi ya mambo ya familia, lakini Diamond hajatumia nafasi hiyo kumzuia kufanya shughuli zake, badala yake amekuwa akimpa sapoti kubwa katika muziki na majukumu mengine ya kikazi.

Zuchu ameeleza kuwa ” “Diamond anapofahamu ana safari au mwaliko wa kwenda kutumbuiza katika eneo fulani, huhakikisha anamsaidia kuweka mazingira mazuri yatakayomwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Amesema jambo hilo ni miongoni mwa vitu anavyovithamini zaidi katika uhusiano wao, akieleza kuwa ushirikiano kutoka kwa mwenzi ni muhimu katika kumwezesha mtu kutimiza ndoto na malengo yake.

Kauli hiyo ya Zuchu inaonesha namna anavyothamini mchango wa Diamond katika safari yake ya muziki, akisisitiza kuwa mafanikio katika uhusiano yanahitaji pia kuelewana, kuaminiana na kupeana nafasi ya kukua katika maeneo mbalimbali ya maisha.

Related Articles

Back to top button