Muziki

Lady Jay Dee ashangazwa na watoto kuimba ‘Yahaya’

MARA:MUZIKI ni sanaa inayoishi kwa muda mrefu, miaka kwa miaka. Msanii nguli wa Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’, ameonesha kushangazwa na watoto kuimba wimbo wake maarufu Yahaya.

Kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii, Lady Jay Dee alishiriki video inayoonesha kundi la watoto wenye umri wa miaka 13 hadi 20 wakiimba kwa hisia wimbo huo, licha ya kuwa umetoka zaidi ya miaka 12 iliyopita.

Kilichomvutia zaidi ni jinsi vijana hao wanavyoyajua maneno ya wimbo huo kwa ufasaha. Akiwa na mshangao, Lady Jay Dee aliandika:

“Katikati ya misa kijana alinifuata akasema Baba Gachuma anakuita. Nikatoka kumsikiliza. Akaniambia panda kwenye gari, akaanza ku-drive sehemu ambayo ni kama pori. Akaniambia leo naenda kukuuza. Akanipeleka hapa kama surprise kwa hawa watoto. Ila najiuliza, Yahaya ina zaidi ya miaka 10, hawa watoto wana miaka mingapi?”

Maneno haya yanaonesha mshangao wake juu ya jinsi Yahaya imeendelea kuishi kupitia vizazi vipya, licha ya kuwa ni wimbo wa zamani.

Nyimbo kama Yahaya ni miongoni mwa kazi zilizomtambulisha Lady Jay Dee kama mmoja wa wasanii wenye mchango mkubwa katika muziki wa Bongo Fleva.

Video hii ni uthibitisho kuwa muziki mzuri huendelea kuishi milele, na kizazi baada ya kizazi kinaendelea kuupokea kwa mapenzi makubwa.

Related Articles

Back to top button