Nyumbani

ZED si wa kubezwa, Azam yaonya

MISRI: AZAM FC imesema haipaswi kuichukulia poa timu ya ZED ya Misri katika mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika, ikieleza kuwa uwezo wa wapinzani hao unaonekana kupitia matokeo yao dhidi ya timu kubwa, ikiwamo Zamalek na Al Ahly.

Akizungumza kabla ya mchezo huo utakaochezwa Ijumaa ya wiki hii, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Azam FC Thabiti Zakaria amesema ZED ni timu yenye ubora na uwezo wa kushindana, hivyo Azam FC inapaswa kujiandaa vizuri ili kupata matokeo mazuri.

Amesema licha ya ZED kutokuwa miongoni mwa timu zinazotajwa sana katika soka la Afrika, kiwango chake kinaonesha kuwa si timu ya kubezwa, hasa baada ya kuifunga Zamalek mabao matatu.

“Matokeo ya mechi moja hayawezi kuonesha kila kitu, lakini nataka upate picha kwamba wanaweza kuifunga timu kama Zamalek mabao matatu. Kwa hiyo si timu ya kubeza,” amesema Zakaria.

Ameongeza kuwa ushindani wa ligi ya Misri na uzoefu wa ZED katika michuano ya kimataifa ni miongoni mwa mambo yanayopaswa kuifanya Azam FC kuwa makini, akibainisha kuwa timu hiyo ina uwezo.

Zakaria amesema Azam FC imeimarika zaidi ikilinganishwa na msimu uliopita, akieleza kuwa kikosi cha sasa kina ubora na kina wachezaji wengi wenye uwezo wa kushindana katika maeneo tofauti ya uwanja.

Akizungumzia ari ya wachezaji kuelekea mchezo huo, Zakaria amesema kikosi kina hamasa kubwa ya kufanya vizuri, hasa baada ya kutafakari makosa yaliyowafanya washindwe kusonga mbele zaidi katika michuano ya Afrika msimu uliopita.

Amesema wachezaji wanatambua umuhimu wa kuanza vizuri tangu mchezo wa kwanza ili kuepuka kurudia makosa ya msimu uliopita, ambapo waliondolewa baada ya kushindwa kutumia vizuri nafasi zao katika hatua ya makundi.

Related Articles

Back to top button