Ligi Kuu

Fikiri ajivunia uimara wa Coastal Union

TANGA: KOCHA wa Coastal Union, Fikiri Elias, amesema bao la mapema lilisaidia timu yake kudhibiti mchezo na kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars.

Fikiri amesema baada ya kupata bao hilo, aliwataka wachezaji wake kucheza kwa mshikamano na nidhamu ili kulinda matokeo na kuhakikisha wanapata pointi tatu muhimu.

Akizungumza baada ya mchezo huo jana amesema wapinzani walibadilisha namna ya kucheza baada ya kufungwa, hali iliyowalazimu kufanya marekebisho ya kiufundi, hasa katika eneo la kiungo na namna ya kuanzisha mashambulizi.

Ameongeza kuwa licha ya changamoto zilizojitokeza katika baadhi ya vipindi vya mchezo, wachezaji wake walionesha kujituma na uimara mkubwa katika safu ya ulinzi, jambo lililowasaidia kudumisha faida yao hadi mwisho.

Kocha huyo amesema ushindi huo una umuhimu mkubwa kwa Coastal Union kwa kuwa unaongeza pointi na kuimarisha kujiamini kwa wachezaji kuelekea michezo inayofuata.

Pia, amewapongeza wachezaji na benchi la ufundi kwa kazi nzuri waliyoifanya, huku akiwashukuru mashabiki waliojitokeza kwa wingi kuisapoti timu na kushuhudia ushindi huo.

Related Articles

Back to top button