Mbeya City yapanga kuzima moto wa kushuka daraja

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga, amesema kikosi chake kimefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye michezo iliyopita kwa lengo la kuongeza ushindani katika mechi zilizosalia za Ligi Kuu.
Mayanga amesema tangu kumalizika kwa mchezo wao wa mwisho kabla ya mapumziko ya Kalenda ya FIFA, benchi la ufundi limeelekeza nguvu katika kuboresha eneo la ulinzi pamoja na umaliziaji wa mashambulizi, maeneo ambayo yalionekana kuhitaji marekebisho.
Mbeya City kwa sasa inaendelea na maandalizi ya mchezo muhimu wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Kocha huyo amesema wachezaji wameonesha ari kubwa mazoezini na wanafahamu umuhimu wa mchezo huo katika harakati za timu kujinasua kutoka eneo la hatari kwenye msimamo wa ligi.
Mbeya City ipo katika presha ya kupambana na kushuka daraja baada ya kujikusanyia pointi 22 pekee na kushika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, hali inayofanya kila mchezo uliosalia kuwa na umuhimu mkubwa kwa mustakabali wa klabu hiyo.
Ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar unaweza kuipa Mbeya City pumzi mpya katika mbio za kusalia Ligi Kuu, huku mashabiki wakitarajia kuona matokeo ya maboresho yaliyofanywa na benchi la ufundi yakionekana uwanjani.




