Katwila: Tumejiandaa kucheza na timu kamili

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Geita Gold Zuberi Katwila amesema mchezo wa kesho dhidi ya Yanga hautategemea uchovu wa wapinzani wao uliotokana na majukumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, badala yake imejiandaa kukabiliana na kikosi hicho ikiwa katika ubora wake.
Katwila amesema Yanga ni miongoni mwa timu kubwa nchini na aina ya mchezo wanaocheza inahitaji maandalizi makini, akisisitiza kuwa hawawezi kuingia uwanjani wakiamini wapinzani wao watakuwa wamechoka.
“Siwezi kusema kuna uchovu kwa Yanga kwa sababu nao wana maandalizi yao na benchi lao la ufundi linajua namna ya kukabiliana na uchovu. Sisi tunajiandaa kucheza na Yanga bila kufikiria kuhusu uchovu wao,” amesema.
Amesema Yanga inapaswa kupewa heshima kutokana na ubora wake, hasa baada ya kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, jambo ambalo limewapa wachezaji wake kujiamini zaidi kuelekea mchezo huo.
Kocha huyo amesema mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na kiwango cha Yanga, lakini wamejipanga kucheza kama timu ili kukabiliana na ubora wa wapinzani wao ambao wana wachezaji wenye uwezo mkubwa mmoja mmoja.




