EPL

Mngqithi: Nafasi tunazopoteza zitatugharimu

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi, amesema timu yake inahitaji kuboresha umaliziaji baada ya takwimu kuonesha inatengeneza nafasi nyingi lakini haifungii kiwango kinachotarajiwa.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Dar es Salaam Leo kuhusu mchezo wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold Mngqithi amesema Yanga inatengeneza wastani wa nafasi 20 kwa kila mchezo, jambo analoliona kuwa ni ishara nzuri, lakini amesisitiza kuwa kutotumia nafasi hizo kunaweza kuja kuwaathiri katika hatua muhimu za msimu, hasa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Bado tunahitaji kuboresha eneo la umaliziaji. Tunatengeneza karibu nafasi 20 kwa mchezo, lakini hatufungi vya kutosha kutokana na nafasi tunazotengeneza,” amesema Mngqithi.

Amesema licha ya Yanga kufunga idadi nzuri ya mabao katika michezo yake ya awali, kiwango cha nafasi kinachopotezwa kinapaswa kuwa tahadhari kwa timu hiyo kutokana na ushindani mkubwa uliopo katika mashindano ya ndani na kimataifa.

Kocha huyo pia ameizungumzia Geita akisema ina kikosi chenye wachezaji wenye uwezo mkubwa mmoja mmoja na pia kinachofanya vizuri kama timu, hivyo Yanga inahitaji maandalizi mazuri na kutumia mapungufu ya mpinzani kupata matokeo.

Mngqithi amesema bado ni mapema kutaja kikosi kitakachoanza kwa kuwa timu haijafanya mazoezi ya kutosha baada ya mchezo uliopita, huku baadhi ya wachezaji wakitarajiwa kuwa na majeraha au maumivu.

Hata hivyo, amesema hafanyi kazi chini ya presha kwa sababu Yanga ipo katika nafasi ambayo amekuwa akiitaka, huku akisisitiza kuwa ligi bado ni ndefu na timu haijakutana na wapinzani wote wakubwa.

Yanga sasa inarejea kwenye ligi baada ya majukumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikitoka kuiondosha Gaborone United kwa jumla ya mabao 3-2.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button