Robertson kuondoka Anfield mwishoni mwa msimu

LIVERPOOL:KLABU ya Liverpool imethibitisha kuwa beki wao wa kushoto na nahodha wa Scotland, Andy Robertson, ataondoka mwishoni mwa msimu huu baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa miaka tisa yenye mafanikio makubwa sana.
Robertson alijiunga na Liverpool akitokea Hull City mwaka 2017, na tangu hapo amekuwa sehemu muhimu ya moja ya vipindi bora zaidi kwenye historia ya kisasa ya klabu hiyo. Katika mechi zake 373 hadi sasa ameifungia Liverpool mabao 13 na asisti 69, akiisaidia timu kushinda mataji mawili ya Premier League, Ligi ya Mabingwa,Kombe la FA, Kombe la ligi mara 2, FIFA Club World Cup, UEFA Super Cup pamoja na Ngao ya Hisani.

Akizungumza wakati wa kuaga, Robertson ametumia maneno ya kugusa akionesha jinsi Liverpool ilivyobadilisha maisha yake.
“Si rahisi kuondoka kwenye klabu kama Liverpool. Imekuwa sehemu kubwa ya maisha yangu na familia yangu kwa miaka tisa iliyopita.”
Ameongeza kuwa licha ya kupata nafasi za kuondoka katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, moyo wake ulimfanya abaki kwa sababu ya upendo mkubwa alionao kwa klabu hiyo.
“Nimeweka moyo na roho yangu yote kwenye klabu hii kwa miaka tisa na sina majuto mengi. Nimekua kama mwanaume na kama mtu. Klabu hii itabaki kuwa dunia yangu.”

Kuondoka kwake kunakuja wakati ambapo nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza imepungua kufuatia ujio wa Milos Kerkez kutoka AFC Bournemouth, jambo lililomfanya kuanza mechi 15 pekee msimu huu.
Kwa mashabiki wengi wa Liverpool, Robertson ataondoka kama mmoja wa mabeki bora zaidi kuwahi kuvaa jezi ya klabu hiyo na sehemu muhimu ya zama za mafanikio chini ya Jürgen Klopp.




