John Legend atangaza albamu ya muziki wa watu Weusi

LOS ANGELES, Marekani: MWANAMUZIKI maarufu wa Marekani, John Legend, ametangaza ujio wa albamu yake mpya ya studio iitwayo ‘Muse’, ambayo inatarajiwa kuachiwa rasmi Oktoba 23, 2026, kupitia lebo ya Republic Records.
Albamu hiyo imetayarishwa kwa ukamilifu na kuandikwa kwa ushirikiano na mtayarishaji na mwanamuziki aliyeshinda tuzo za Grammy, Pharrell Williams, ikiwa ni mara ya kwanza kwa wawili hao kufanya kazi pamoja kwa kiwango hicho baada ya zaidi ya miaka 20 ya urafiki wao.
‘Muse’ imeelezwa kuwa kazi ya kipekee inayochanganya aina mbalimbali za muziki wa watu weusi, ikiwemo Gospel, Soul, Doo-wop, Afrobeat na Hip-hop, huku ikiwa na ladha ya kisasa na mpangilio wa kimuziki wenye taswira ya kifahari na ya kisanaa.
Sambamba na kutangaza albamu hiyo, John Legend ameachia wimbo wake mpya unaoitwa ‘Daylight’, ambao aliutumbuiza kwa mara ya kwanza wakati wa kipindi maalumu cha America’s Tailgate kilichoandaliwa na CBS kuelekea kuanza kwa msimu mpya wa NFL.

Legend amesema albamu hiyo inalenga kuvunja mtazamo wa kazi zake za awali ambazo zimekuwa zikihusishwa zaidi na nyimbo za piano zenye hisia. Kwa mujibu wa msanii huyo, alitaka kufanya jambo jipya ambalo lingemshangaza yeye mwenyewe pamoja na mashabiki wake.
Ushirikiano wa Legend na Pharrell ulianza kuchukua sura baada ya Legend kushiriki katika albamu ya Clipse, Let God Sort ‘Em Out, iliyotayarishwa na Pharrell. Baada ya kusikia sauti ya Legend kwenye wimbo ‘The Birds Don’t Sing’, Pharrell alipata wazo la kutengeneza albamu nzima.
Wawili hao walianza kurekodi na kuandika nyimbo za ‘Muse’ jijini Paris, Ufaransa, Januari 2025. Albamu hiyo imechota msukumo kutoka kwa wasanii wakubwa kama Nina Simone, Nat King Cole na Marvin Gaye, huku ikichanganya muziki wa zamani na midundo ya kisasa.
Kwa upande wake, Pharrell ameeleza dhamira ya kutengeneza kazi yenye ladha ya kisasa lakini inayobeba vipengele vya muziki wa zamani. Albamu hiyo pia imehusishwa na wimbo ‘Pray For Ya’, ambao uliwahi kutumika katika maonesho ya ‘Louis Vuitton Fall-Winter 2026 Men’s Show’.
‘Muse’ pia imebeba simulizi kuhusu mapenzi, tamaa, kujitoa na usaliti, huku wimbo wa kichwa cha albamu ukimzungumzia mwanamume na mwanamke anayekuwa chanzo cha msukumo wake wa kisanaa.
John Legend amesema jina ‘Muse’ pia linarejea katika dhana ya Muses wa mitholojia ya Kigiriki miungu wa kike waliokuwa wakihusishwa na muziki, sayansi, fasihi na sanaa.
Kwa mashabiki wa John Legend, albamu hiyo inatarajiwa kuwa sura mpya katika safari yake ya muziki, huku ushirikiano wake na Pharrell Williams ukitarajiwa kuleta mchanganyiko wa kipekee kati ya sauti yake ya soulful na ubunifu wa Pharrell.



