Nyumbani

Mwalimu: Yanga mmenipa heshima

DAR ES SALAAM: MCHEZAJI wa Yanga, Selemani Mwalimu, amesema amefurahishwa na heshima aliyopewa na klabu hiyo ya kumtengenezea siku maalumu ya mchezaji, akisema hajawahi kupata heshima ya aina hiyo katika kipindi chake cha kucheza soka.

Mwalimu amesema tukio hilo limempa furaha kubwa na kumfanya azidi kuthamini uhusiano wake na Yanga, huku akiwashukuru viongozi wa klabu hiyo kwa heshima hiyo.

“Ninafuraha kwa timu kunipa siku maalumu ya mchezaji. Ni heshima ambayo timu imenipa. Hapo awali sijawahi kupata heshima kama hii, kwamba kuna siku yangu maalumu ambayo timu imenipa. Kwa hiyo napenda kumshukuru Mungu na pia kuwashukuru viongozi wa Yanga kwa heshima hiyo walionipa,” amesema Mwalimu.

Mchezaji huyo amesema pia anatarajia kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana kesho, akisisitiza kuwa mafanikio yake katika mchezo uliopita yalitokana na ushirikiano wa wachezaji wenzake.

“Ni matamanio na matarajio ya kila mchezaji kupambana kwa ajili ya timu yake. Napenda kumshukuru Mungu kwa mechi ya Gaborone. Nilipata nafasi ya kufanya vizuri katika mechi ile, lakini kushirikiana na wenzangu ndiyo maana nikapata ‘performance’ kama ile,” amesema.

Kwa upande wake, nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto, amesema kikosi hicho kina morali kubwa kuelekea mchezo huo, huku kila mchezaji akiwa tayari kupambana endapo atapewa nafasi.

“Wachezaji tuna morali kubwa na kama unavyoona, malengo ya timu ni kufika mbali. Timu ina kikosi kikubwa na kila mchezaji ambaye ataaminiwa na kupewa nafasi atapambana kwa ajili ya timu ili kupata matokeo mazuri,” amesema Mwamnyeto.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button