Gabo aongeza ujuzi wa filamu kutangaza utalii Beijing

CHINA: NYOYA wa filamu nchini, Salim Ahmed Issa, maarufu kwa jina la Gabo Zigamba, amehitimu mafunzo maalumu ya siku 14 yaliyolenga kuwajengea washiriki uwezo wa kutumia filamu katika kutangaza historia, utalii na utamaduni.
Mafunzo hayo yalifanyika jijini Beijing, China, katika Akademia Kuu ya Utamaduni na Utalii ya China, ambapo Gabo alipokea cheti cha ushiriki baada ya kukamilisha programu hiyo.
Mbali na Gabo, Tanzania pia iliwakilishwa na Omari Simbano, mtumishi wa Bodi ya Filamu Tanzania. Ushiriki wao uliratibiwa na Bodi ya Filamu Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, chini ya Wizara ya Biashara ya China.
Mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha washiriki kutumia sanaa ya filamu kama nyenzo muhimu ya kutangaza historia, vivutio vya utalii na utamaduni wa mataifa yao, sambamba na kukuza ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya utamaduni na ubunifu.
Bodi ya Filamu Tanzania, chini ya Katibu Mtendaji wake, Dkt. Gervas Kasiga maarufu kama Chuma, imeendelea kuimarisha diplomasia ya kisekta na ushirikiano na China.
Kwa kipindi cha mwaka mmoja, jumla ya wanatasnia wa filamu na watumishi wanane wamepata fursa ya kushiriki mafunzo ya muda mfupi na mrefu nchini China kupitia ushirikiano huo.
Juhudi hizo zinaelezwa kuwa ni mwendelezo wa mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati ya Tanzania na China, yaliyojengwa na viongozi wa nchi hizo mbili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping.
Aidha, katika kipindi cha mwaka mmoja pekee, Bodi ya Filamu Tanzania imefanikiwa kutengeneza nafasi 30 za mafunzo kwa wanatasnia wa filamu na michezo ya kuigiza, hatua inayowawezesha kupata ujuzi na uzoefu wa kisekta kutoka katika mataifa mbalimbali duniani.
Hatua hiyo inatajwa kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uwezo wa wataalamu wa filamu nchini, huku ikifungua fursa zaidi za kuitangaza Tanzania kupitia filamu, utalii, historia na utamaduni wake.
Kupitia mafunzo ya aina hiyo, wanatasnia wa filamu wanatarajiwa kutumia maarifa waliyoyapata kuboresha kazi zao na kushiriki kikamilifu katika kuitangaza Tanzania ndani na nje ya nchi.



