Clara Luvanga atimkia Washington Spirit

WASHINGTON: KLABU ya Washington Spirit ya Marekani imetangaza kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Clara Luvanga kwa mkataba wa miaka minne.
Washington imemsajili Clara kutoka Al-Nassr ya Wanawake ya Saudi Arabia aliyodumu nayo kwa misimu mitatu ya mafanikio.
Clara ambaye ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza Ligi ya NWSL ya Marekani, anatajwa kusajiliwa kwa kitita cha Pauni milioni 2.
Kupitia akaunti ya Mtandao wa Instagram ya Washington, ilimkaribisha Clara kwa kuandika: “Hatua mpya. Karibu DC, Clara! Tumemsajili Clara Luvanga kwa mkataba wa miaka minne, utakaodumu hadi mwisho wa msimu wa 2029.”
Nyota huyo, 21 anaondoka Al-Nassr baada ya kuipa timu hiyo ndoo ya Saudi Women’s Premier League mara tatu mfululizo.
Pia, ameipa timu hiyo makombe ya Women Super Cup kwa misimu miwili mfululizo na msimu uliopita alitwaa kiatu cha dhahabu cha ligi baada ya kufunga mabao 24.
Al-Nassr imemuaga mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga Princess kwa kuandika Instagram: “Kwaheri Clara. Kumbukumbu zitasalia daima. Asante kwa kila kitu, na kwa kila kumbukumbu.”




