Muziki

Lady Jaydee, H Baba na Prezzo kuongoza miaka 30 ya Bongo Fleva Mwanza

MWANZA: WASANII wakongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura maarufu Lady Jaydee, H Baba na Prezzo ni miongoni mwa mastaa watakaotumbuiza katika tamasha la maadhimisho ya miaka 30 ya Bongo Fleva litakalofanyika Agosti 8, 2026, jijini Mwanza.

Mashambulizi ya burudani sasa yamehamia jijini Mwanza, huku maandalizi ya tamasha hilo yakizidi kushika kasi baada ya waandaaji kutangaza kuongezwa kwa wasanii hao waliotoa mchango mkubwa katika ukuaji wa muziki wa Bongo Fleva.

Tamasha hilo linatarajiwa kuwakutanisha maelfu ya mashabiki wa muziki kutoka Mwanza na mikoa jirani kushuhudia burudani kutoka kwa baadhi ya wasanii walioweka historia katika tasnia ya muziki nchini.

Mbali na Lady Jaydee, H Baba na Prezzo, wasanii wengine watakaopanda jukwaani ni AY, Fid Q, Chege, Juma Nature, Temba, Jay Moe, Soggy Doggy, Jaffary, Ferooz, Daz Baba, Moxie, Tunda Man, Madee, KR, Mr Blue, Dully Sykes, Joslin, Kalapina, Domokaya, Luten Kalama, Q Chief, 20 Percent, Lord Eyez, Rado, Mwasiti, Stara Thomas, Keisha, King Crazy GK, Solid Ground, Dudu Baya, Matonya, Baraka Da Prince, Mabaga Fresh na Mwana FA.

Tamasha hilo linaendelea kuwa sehemu ya maadhimisho ya kutimiza miaka 30 ya Bongo Fleva, likiwa na lengo la kutambua mchango wa wasanii walioasisi na kuendeleza muziki huo pamoja na kuwakutanisha mashabiki wa kizazi cha zamani na cha sasa katika usiku wa kumbukumbu na burudani.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button