Sowah arejea Singida Black Stars

SINGIDA: Baada ya msimu mmoja usio na mafanikio akiwa Simba SC, mshambuliaji raia wa Ghana, Jonathan Sowah, amerejea Singida Black Stars kwa mkataba wa miaka mitatu akilenga kufufua kiwango chake.
Singida Black Stars imethibitisha kurejea kwa mshambuliaji huyo aliyewahi kuwa tegemeo la safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kabla ya kuhamia Simba mwanzoni mwa msimu uliopita.
Akiwa Simba, Sowah alishindwa kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza kutokana na ushindani mkubwa wa namba na changamoto za kiwango, hali iliyomfanya acheze mechi chache na baadaye kutokuwa sehemu ya mipango ya benchi la ufundi.
Kurejea kwake kunatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Singida Black Stars kuimarisha safu ya ushambuliaji kuelekea msimu mpya wa mashindano ya ndani na kimataifa, huku klabu ikiamini uzoefu wake utaongeza makali ya timu.
Sowah anarejea katika mazingira anayoyafahamu vizuri, akiwa na jukumu la kurejesha makali yake ya kufunga mabao na kuisaidia Singida Black Stars kutimiza malengo yake katika msimu wa 2026/27.




