Ligi Kuu

Kiboko ya Azam Fc mikononi mwa Mashujaa

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Salum Mayanga, ni miongoni mwa makocha wanaojadiliwa na uongozi wa timu ya Mashujaa FC kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Mohammed Abdallah “Bares” kama kocha mkuu wa kikosi hicho.

Mayanga, ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Mbeya City, hivi karibuni aliiongoza timu hiyo kuitoa Azam FC kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB kwa mikwaju ya penalti 4-2, baada ya kutoka sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Taarifa kutoka ndani ya Mashujaa FC zinaeleza kuwa jina la Mayanga limekuwa likitajwa mara kwa mara katika vikao vya uongozi wa timu hiyo, wakiamini kuwa anaweza kuwa msaada mkubwa katika malengo yao.

“Hatujaanza mazungumzo rasmi na kocha yeyote, lakini kuna majina tunayojadili, na Mayanga ni mmoja wao. Amejadiliwa sana kama chaguo linalofaa kuchukua nafasi ya Bares,” kilisema chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.

Kwa upande wake, Mayanga amesisitiza kuwa hajafanya mazungumzo na timu yoyote na kwa sasa anabaki na Mbeya City, akiendelea kuandaa kikosi chake kwa michezo ya Championship.

“Hakuna kiongozi wa Mashujaa FC aliyewasiliana nami au kuanzisha mazungumzo yoyote. Siwezi kupinga kama wananijadili, lakini kwa sasa niko Mbeya City. Tumewasili jana kutoka Dar es Salaam baada ya mchezo wetu dhidi ya Azam FC,” amesema Mayanga

Related Articles

Back to top button