
DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva na mwigizaji Irene Uwoya amesema kuwa hana tabia ya kuwa na migogoro na watu, akisisitiza kuwa yeye ni mtu wa upendo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Irene aliandika kuwa iwapo mtu ataonekana kuwa na shida naye, basi huenda ametumia muda na nguvu nyingi kutengeneza mgogoro huo.
“Mimi sina shida na mtu, nina upendo sana. Ila ukiona mtu ana shida na mimi, jua ametumia nguvu sana na muda wa kutosha kuitafuta hiyo shida,” ameandika Irene.
Mbali na hilo, Irene pia amezungumza kuhusu siri ya kuendelea kuonekana mwenye ujana na mrembo kila siku.
Akijibu swali hilo, aliloulizwa na msanii Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’ katika sherehe ya kumbukizi ya kuzaliwa ya Mama Diamond anayeitwa Sandra akitimiza miaka 59amesema kuwa hana siri yoyote ya kipekee, bali ni neema ya Mungu inayomuwezesha kuendelea kung’aa.
Kauli yake imeibua mijadala miongoni mwa wafuasi wake, huku wengi wakimpongeza kwa msimamo wake wa kuhimiza upendo na kumshukuru Mungu kwa kila jambo.




