Yanga yapigwa faini ya Sh milioni 100, Hersi apelekwa Kamati ya Maadili

DAR ES SALAAM:BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imeitoza Yanga faini ya Sh milioni 100 na kuwapeleka Rais wa klabu hiyo, Hersi Said, pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu, Andre Mtine, katika Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kufuatia ukiukaji wa kanuni za matumizi ya vyumba vya kubadilishia nguo.
Uamuzi huo ulifikiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi katika kikao chake kilichofanyika Julai 2, 2026, baada ya kupitia matukio mbalimbali ya Ligi Kuu ya NBC.
Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB, Yanga ilikiuka Kanuni ya 17:20 ya Ligi Kuu baada ya wachezaji na benchi la ufundi kutotumia chumba rasmi cha kuvalia katika mchezo namba 233 dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, na badala yake kutumia nyumba iliyopo nje ya uwanja upande wa pili wa barabara.
TPLB ilieleza kuwa adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 27:7 ya Ligi Kuu kuhusu Vyombo vya Maamuzi.
Aidha, Hersi na Mtine wameitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya TFF kutoa maelezo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni ukiukaji wa kanuni unaojirudia, baada ya Yanga pia kutozwa faini ya Sh milioni 30 mwezi Mei mwaka huu kwa kosa kama hilo.
Katika maamuzi mengine, Klabu ya Mtibwa Sugar imetozwa faini ya Sh milioni 5 kwa kutotumia chumba rasmi cha kuvalia kwenye mchezo dhidi ya Namungo FC uliochezwa Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi.
Kwa upande wa KMC, klabu hiyo imepewa onyo kali baada ya wachezaji wake watatu kuvaa jezi zenye namba zinazozidi 70, jambo lililokiuka kanuni za Ligi Kuu.
Wakati huo huo, TPLB imechukua hatua kali dhidi ya Stand FC Masasi baada ya kubaini udanganyifu wa usajili katika mchezo wa mchujo wa First League dhidi ya Pan African FC.
Mchezaji Ramadhani Bakari Mlaponi amefungiwa miezi 12 kwa kutumia leseni ya mchezaji mwingine, huku Stand FC ikinyang’anywa ushindi wake wa mabao 1-0 na Pan African kupewa ushindi wa mabao 3-0.
Pia, kocha wa Stand FC, Mbano Kizito, amefungiwa kwa miezi 12 na kutozwa faini ya Sh 500,000 kwa kumchezesha mchezaji ambaye hakuwa halali kwa mujibu wa kanuni za usajili.




