Simeone: Julián Álvarez ndiye mchezaji bora tuliyenaye Atlético

MADRID:KOCHA wa Atlético Madrid, Diego Simeone, amezungumzia kwa mara ya kwanza mustakabali wa Julián Álvarez tangu mshambuliaji huyo aombe kuondoka katika klabu hiyo majira haya ya joto.
Akizungumza na ESPN, Simeone alimwaga sifa kwa nyota huyo wa Argentina na kueleza kuwa ni mchezaji muhimu sana ndani ya kikosi chake.
“Julián ni mchezaji wa ajabu. Kwangu, ndiye mchezaji bora tuliyenaye Atlético. Sina chochote cha kusema zaidi ya mazuri kuhusu yeye. Ni mchezaji wa kiwango cha juu na kupata mtu wa aina yake si jambo rahisi,” amesema Simeone.
Alipoulizwa kuhusu hatma ya mshambuliaji huyo, Simeone alikwepa kutoa majibu ya moja kwa moja na kusisitiza kuwa kwa sasa akili ya Álvarez inapaswa kuwa kwenye Kombe la Dunia akiwa na Argentina.
“Kwa sasa mechi inayofuata ya Julián ni akiwa na Argentina. Anatakiwa afikirie hilo kwanza. Baada ya hapo, mambo mengine yatajipanga kama yanavyojipanga siku zote maishani,” ameongeza kocha huyo.
Kauli ya Simeone imekuja wakati tetesi zikizidi kuhusisha Álvarez na kuondoka Atlético Madrid, huku klabu kadhaa kubwa barani Ulaya zikitajwa kufuatilia hali yake.




