Ibenge: Simba ni timu imara, lakini tupo tayari kutwaa ubingwa

ZANZIBAR:KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema kikosi chake kipo tayari kwa pambano la fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Simba, akisisitiza kuwa wanaiheshimu timu hiyo lakini wanaingia uwanjani kwa lengo la kutwaa ubingwa.
Ibenge amesema Simba ni moja ya timu bora nchini, hivyo mchezo huo utahitaji maandalizi makubwa ya kiufundi na nidhamu ya hali ya juu kutoka kwa wachezaji wake.
“Simba ni timu nzuri na yenye ubora. Tunafahamu ubora wao, lakini sisi pia tumefanya maandalizi yetu. Katika fainali hakuna nafasi ya kufanya makosa mengi,” amesema Ibenge.
Kocha huyo raia wa DR Congo amesema uzoefu wa kucheza mechi kubwa utakuwa muhimu, lakini matokeo yataamuliwa na namna timu itakavyotekeleza mpango wa mchezo ndani ya dakika 90 au zaidi.
Ameongeza kuwa Azam FC haitaingia uwanjani ikiwa na presha ya matokeo ya mechi zilizopita, badala yake itaangalia fainali hiyo kama mchezo mpya wenye umuhimu wa kipekee.
“Tunahitaji kucheza kwa utulivu, nidhamu na kutumia vizuri nafasi tutakazozipata. Hiyo ndiyo njia ya kufikia lengo letu la kutwaa kombe,” alisema.
Fainali hiyo itawakutanisha makocha wawili wenye uzoefu mkubwa barani Afrika, Ibenge wa Azam FC na Steve Barker wa Simba, katika pambano linalotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.




