Nyumbani

TPC yaanza Mbio za Los Angeles

DAR ES SALAAM: KAMATI ya Paralympic Tanzania (TPC) imekamilisha rasmi safu yake ya uongozi baada ya kufanya uchaguzi mdogo uliojazwa nafasi zilizoachwa wazi, huku viongozi wapya wakitakiwa kuanza kazi mara moja kwa lengo la kuongeza ushiriki wa Tanzania katika Michezo ya Paralympic ya Los Angeles 2028.

Katika uchaguzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Dk (CPA) Zelia Njeza alichaguliwa kuwa Mweka Hazina mpya baada ya kupata kura 11, wakati Ramadhan Namkoveka akichaguliwa kuwa Katibu Mkuu mpya kwa kupata kura tisa za ndiyo, kura moja ya hapana na mjumbe mmoja kujizuia kupiga kura.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo, Rais wa TPC, Tuma Dandi, amesema kukamilika kwa safu ya uongozi kunafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya michezo ya watu wenye ulemavu nchini.

Dandi amesema viongozi hao wapya wanapaswa kuingia kazini kwa kasi kubwa ili kusaidia utekelezaji wa malengo ya TPC ya kukuza michezo ya walemavu na kuongeza uwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.

“Sasa TPC imekamilika. Tunatakiwa kufanya kazi kwa kasi kubwa ili kuleta maendeleo ya haraka kwa maslahi ya watu wenye ulemavu. Lengo letu kuu ni kuhakikisha kuwa katika Michezo ya Paralympic ya Los Angeles, Tanzania inapeleka wachezaji wengi zaidi na katika michezo mingi zaidi,” amesema Dandi.

Ameongeza kuwa uzoefu wa Michezo ya Paralympic ya Paris, Ufaransa, ambapo Tanzania ilishiriki mchezo mmoja wa mbio za baiskeli za viti mwendo pekee, unapaswa kuwa chachu ya kuongeza juhudi za kuibua vipaji na kuandaa wanamichezo wengi zaidi.

Uchaguzi huo ulisimamiwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia Ofisa Michezo Mwandamizi, Ingrid Kimario, na ulihudhuriwa na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TPC pamoja na wawakilishi wa vyama mbalimbali vya michezo ya watu wenye ulemavu nchini.

Miongoni mwa vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo ni Tanzania Para Swimming Association, Tanzania Wheelchair Basketball Association, Tanzania Goalball Association, Tanzania Para Volleyball Association, Tanzania Para Powerlifting Association, Tanzania Para Athletics pamoja na Kamati ya Paralympic Mkoa wa Iringa.

TPC imeeleza kuwa kukamilika kwa uchaguzi huo ni hatua muhimu ya kuimarisha utawala wa michezo ya walemavu nchini na kuweka msingi wa mafanikio makubwa katika mashindano ya kimataifa yanayokuja.

Related Articles

Back to top button