TRA United na Coastal Union zapania pointi tatu Arusha

ARUSHA: TRA United itakuwa nyumbani kesho Juni 24, 2026 kuikaribisha Coastal Union katika mchezo wa Ligi Kuu, huku kila timu ikiingia uwanjani ikiwa na dhamira ya kuondoka na pointi tatu muhimu.
Kocha wa TRA United, Etienne Ndayiragije, amesema maandalizi ya timu yake yamekamilika na kikosi kipo tayari kwa mchezo huo. Amesema kurejea kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa nje kutokana na majeraha kumeongeza nguvu na chaguo zaidi ndani ya timu.
Kwa upande wake, kiungo Ramadhan Salum ‘Chobwedo’, amesema watautumia vyema uwanja wa nyumbani kutafuta ushindi utakaowapa matumaini ya kumaliza msimu katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi.
“Tumejiandaa kupeleka ushindani mkubwa na kuhakikisha tunapata matokeo mazuri mbele ya mashabiki wetu,” amesema Chobwedo.
Kwa Upande wa Coastal Union, Kocha Fikiri Elias amesema kikosi chake kimejiandaa vizuri kwa mchezo huo na wachezaji wamezoea hali ya hewa ya Arusha, jambo ambalo linaongeza imani ya kufanya vizuri.
Amesema lengo la timu yake ni kucheza soka la kuvutia na kupambana kuhakikisha inaondoka na alama zote tatu.
Naye mchezaji wa Coastal Union, Luician Kilua, amesema wachezaji wote wako katika hali nzuri na ari kubwa ya kuzipigania pointi tatu muhimu katika mchezo huo.




