Huyu mwandishi wa habari hatakuja kusahau hii siku

TEXAS:USHINDI wa Argentina dhidi ya Austria katika Kombe la Dunia 2026 ulileta furaha kubwa kwa mashabiki wa Albiceleste, lakini pia ulimzawadia mwandishi mmoja wa habari kumbukumbu ambayo huenda akaisimulia maisha yake yote.
Mwandishi wa TyC Sports, Joaquín Bruno, alijikuta katikati ya tukio la kipekee baada ya Lionel Messi kufunga bao la pili lililoihakikishia Argentina ushindi na nafasi katika hatua ya 32 bora.
Bruno alikuwa amesimama nyuma ya goli akifuatilia mchezo huku mwenzake akiwa tayari ameondoka kuelekea eneo la mahojiano baada ya mechi.
Dakika za mwisho za mchezo zilikuwa na presha kubwa. Kwanza, shuti la Julián Álvarez liliokolewa na kipa wa Austria. Mpira ulipomfikia Messi, jaribio lake la kwanza lilizuiwa. Hata hivyo, katika nafasi ya pili, nahodha huyo wa Argentina hakufanya makosa na kupeleka mpira wavuni.
Bruno anasema alishangilia bao hilo kwa nguvu kama shabiki wa kawaida.
“Nilipiga kelele kama mwendawazimu. Nilikuwa karibu sana na tukio hilo. Kisha nikamuona Messi akija upande wangu. Nilikuwa bado nashangilia na ghafla akaanza kuniangalia. Alinisogelea na kunipa high five,” ameeleza Bruno.

Mwandishi huyo amesema bado anaona vigumu kuelezea hisia alizopata katika sekunde hizo chache.
Kwa mtu ambaye amekuwa akimfuatilia Messi kwa miaka mingi na ambaye ni shabiki mkubwa wa Argentina, kugusana na nahodha huyo katika wakati wa kihistoria ilikuwa jambo lisilotarajiwa.
Dakika chache baada ya tukio hilo, simu yake ilianza kupokea mamia ya ujumbe kutoka kwa marafiki, familia na mashabiki waliokuwa tayari wameona picha hiyo ikisambaa duniani.
Katika Kombe la Dunia ambalo limejaa mabao, rekodi na matukio makubwa, kwa Joaquín Bruno, hakuna kitakacholingana na sekunde chache ambazo Lionel Messi alisimama mbele yake na kushiriki naye furaha ya ushindi.



