Kuogelea

TPC yazindua mashindano ya Taifa ya Paralimpiki

DAR ES SALAAM: KAMATI ya Paralimpiki Tanzania (TPC) imezindua rasmi mashindano ya Taifa ya watu wenye Ulemavu, yatakayokuwa msingi wa kuibua vipaji na kuandaa timu ya taifa kwa ajili ya Michezo ya Paralimpiki ya Los Angeles 2028 nchini Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa TPC, Ramadhan Namkoveka, uamuzi huo wa kihistoria umeidhinishwa na Kamati ya Utendaji ya TPC kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya michezo ya watu wenye ulemavu nchini na kuongeza ushindani wa kimataifa.

Namkoveka amesema TPC itaandaa mashindano matatu makubwa ya kitaifa mwaka 2026. Mashindano ya kuibua vipaji vya kuogelea kwa watu wenye ulemavu yatafanyika Oktoba 10, huku mashindano ya Taifa ya mpira wa kikapu kwa watumiaji wa viti mwendo yakifanyika Novemba 21.

Mashindano makuu ya Tanzania National Para Games, yatakayohusisha riadha, powerlifting, mbio za viti mwendo na goalball, yanatarajiwa kufanyika Novemba 28 jijini Dar es Salaam.

Namkoveka amesema maeneo ya kufanyikia mashindano hayo yanaendelea kuratibiwa kwa kushirikiana na mamlaka husika na taarifa zaidi kuhusu utaratibu wa mashindano hayo itatolewa baada ya kukamilika kwa maandalizi ya mwisho.

Kwa mujibu wake, TPC imezitaka chama cha michezo ya watu wenye ulemavu ngazi ya taifa na mikoa Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na wadau wengine kuanza mara moja maandalizi ya timu na mazoezi ya wanamichezo wao.
Ameeleza kuwa mashindano hayo yatakuwa nguzo muhimu ya safari ya kuelekea Paralimpiki ya Los Angeles 2028, ambapo wanamichezo watakaofanya vizuri watapata nafasi ya kushiriki mashindano ya dunia kwa ajili ya kupata hadhi ya kimataifa ya uainishaji na hatimaye kufuzu kuiwakilisha Tanzania.

Katika hatua nyingine, TPC imeeleza dhamira yake ya kuhakikisha watu wote wenye ulemavu wanapata fursa ya kushiriki michezo na kwamba inaendelea kuweka mifumo ya kuvishirikisha vyama mbalimbali vya michezo ili kupanua wigo wa ushiriki katika mashindano hayo.

Dirisha rasmi la kupata uainishaji wa kimataifa na kufuzu mashindano hayo lilifunguliwa Januari 1, 2026 na litafungwa Julai 2, 2028.

“Tushirikiane kuleta mapinduzi na heshima ya nchi katika michezo ya watu wenye ulemavu nchini,” amesema Namkoveka.

 

Related Articles

Back to top button