Ligi Kuu

‘Simba tunautaka ubingwa wa shirikisho’ Ahmed

ARUSHA: WEKUNDU wa Msimbazi Simba wamesema wanautaka ubingwa wa Kombe la Shirikisho.

Kauli hiyo imetolewa na Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, mkoani Arusha ambapo Simba tayari imetua huko kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali wa kombe la shirikisho dhidi ya Coastal Union unaotarajiwa kuchezwa kesho.

Akizungumza na wanachama na mashabiki wa Simba wa Mererani, Ahmed amesema Simba imewahi kuishia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho mara tatu katika mikoa tofauti, lakini anaamini safari hii mambo yatakuwa tofauti kutokana na sapoti ya mashabiki wa Arusha.

“Tulishashindwa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho mara tatu. Tulicheza Mwanza tukapoteza, tukapoteza Mtwara, tukapoteza Manyara lakini sasa ni Arusha. Arusha hamjawahi kutuangusha. Tunaamini kwa ushirikiano Jumamosi tutakwenda fainali,” amesema

Amesema kuwa Simba bado inapigania mataji mawili makubwa msimu huu, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, akieleza kuwa ubora wa kikosi walichonacho unawapa imani ya kufikia malengo hayo.
Ahmed pia aligusia mwenendo wa Ligi Kuu, akidai kuwa baadhi ya matukio yaliyotokea msimu huu yameathiri safari ya timu yao katika mbio za ubingwa, huku akieleza kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliohusika.

Mbali na masuala ya uwanjani, Ahmed aliwahamasisha Wanasimba wa Mererani kujiandaa kuchukua kadi za uanachama mara zitakapoanza kutolewa rasmi, akiahidi kufika kuzindua tawi la Simba katika eneo hilo.

Related Articles

Back to top button