Kapombe ataja siri waliyotumia kwa Mbeya City

DAR ES SALAAM: NAHODHA wa Simba SC, Shomari Kapombe, amesema kilichowapa ushindi kwa Mbeya City ni umakini na tahadhari.
Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya timu hiyo inayotetea nafasi ya kujinusuru isishuke daraja, mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya jana.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kapombe, amesema timu yake ilicheza kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha inaondoka na pointi tatu jambo lililofanikiwa.
Kapombe amesema Simba ilianza mchezo kwa kasi kubwa huku ikishambulia kwa nguvu katika dakika za mwanzo kabla ya kuzingatia kulinda bao ililopata.
“Tulicheza kwa tahadhari kubwa na hata tulipopata kila goli tulikuwa tunalinda huku tunaendelea kutafuta lingine. Dakika ya kwanza mpaka ya 20 presha ilikuwa juu. Tulikuwa tunashambulia huku tunadumisha tulichopata kwa sababu muhimu ilikuwa ni pointi tatu,” amesema Kapombe.
Nahodha huyo amesisitiza kuwa ushindi huo ni muhimu katika mbio za timu hiyo za kutimiza malengo yake msimu huu.
Wekundu hao wameanza safari ya kulekea mkoani Arusha kwa ajili ya mchezo ujao.




