Ni Mo Salah au De Bruyne leo?

SEATTLE:KATIKA mchezo wa leo unaowakutanisha miamba wawili wa soka kutoka Afrika na Ulaya, kila mmoja akitamba katika anga zake,wakati Ubelgiji ikiwa ni taifa bora barani Ulaya na Misri ikiwa dume la soka Afrika,ndani yao zipo stori zinazofanana kutoka kwa wanaume wawili wakubwa wa soka la dunia.
Mohamed Salah na Kevin De Bruyne, wote wakiwa na miaka 34, wanakutana leo katika mchezo pekee kuwahi kuwakutanisha kwenye Kombe la Dunia, wakiwa kwenye ncha za mwisho za safari yao ya soka la ushindani.
Licha ya wote kuwa mastaa wakubwa katika soka la England kwa nyakati tofauti, wamepitia safari zinazofanana. Mohamed Salah aliyeondoka Ligi Kuu ya Misri baada ya mapinduzi ya 2011 yaliyosimamisha michezo kwa muda, alijikuta mikononi mwa Chelsea mwaka 2014 baada ya kucheza misimu kadhaa katika FC Basel.
Maisha yake ndani ya Chelsea chini ya Jose Mourinho hayakuwa rahisi kutokana na ushindani mkubwa wa kikosi, akifanikiwa kufunga mabao mawili pekee katika mechi 19 kabla ya kutolewa kwa mkopo kwenda Fiorentina, na baadaye kuuzwa moja kwa moja kwenda AS Roma ambako alirejea kwenye ubora wake na hatimaye kurudi EPL.
Upande mwingine, De Bruyne alisajiliwa na Chelsea kama kiungo kinda akitokea Ubelgiji, lakini hakupata nafasi chini ya Mourinho, akicheza mechi tisa pekee kabla ya kupelekwa Wolfsburg kwa mkopo na baadaye kuuzwa moja kwa moja.
Nyota hawa waligeuka kuwa lulu nje ya Chelsea. Salah aling’ara Fiorentina na Roma hadi kuwashawishi Liverpool kumsajili, huku De Bruyne aking’ara Wolfsburg na baadaye kurejea England kupitia Manchester City.
Baada ya kurejea England, kila mmoja aliandika historia yake,Salah akiisaidia Liverpool kutwaa mataji mawili ya EPL baada ya miaka 30 ya ukame na kucheza fainali tatu za UEFA Champions League, akibeba taji moja. Kwa upande wa De Bruyne, ametwaa mataji sita ya EPL na kusaidia Manchester City kushinda UEFA Champions League kwa mara ya kwanza.
Kwa timu za taifa, wote hawajawa na mafanikio makubwa. Salah hajawahi kutwaa taji na Misri, mafanikio yake makubwa yakiwa kufika fainali mbili za AFCON (2017 na 2021), huku De Bruyne akifikia nusu fainali ya Kombe la Dunia 2018 akiwa na Ubelgiji.
Wawili hawa wanakutana leo katika mchezo unaoweza kuwa wa mwisho kwao kukutana kimataifa, wakati ambao wote wameondoka EPL,De Bruyne akimalizia soka lake Napoli, na Salah akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake Liverpool.




