UEFA yatupa kete UEFA 2029

BARCELONA:DIMBA la Camp Nou limeingia rasmi kwenye kinyang’anyiro cha kuandaa fainali ya UEFA Champions League ya mwaka 2029, baada ya zoezi la maombi kufikia hatua ya mwisho. Kwa sasa viwanja viwili tu ndivyo vimebaki, na mshindi atajulikana Septemba 15 huko Thessaloniki, Ugiriki.
Wamiliki wa uwanja huo, FC Barcelona, wanapiga hesabu za kumaliza maboresho makubwa kabla ya 2029, ambapo Camp Nou inatarajiwa kubeba mashabiki zaidi ya 104,000, huku sehemu ya VIP ikiwa na watu karibu 9,000. Hii itaifanya iwe moja ya viwanja vikubwa na vya kisasa zaidi Ulaya.
Ombi lao linaungwa mkono na serikali ya Hispania, Katalunya pamoja na shirikisho la soka la nchi hiyo, hasa wakijiandaa pia na Kombe la Dunia 2030. Hata hivyo, kuna upinzani mkali kutoka uwanja wa Wembley, na pia UEFA inaweza kuangalia suala la Hispania kupewa fainali mara mbili karibu, kwani mwaka 2027 itachezwa katika dimba la Metropolitano.
Kumbukumbu zinaonesha mara ya mwisho Camp Nou kuandaa fainali ilikuwa 1999, ambapo Manchester United walichukua ubingwa kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Bayern Munich. Sasa macho yote yanaangalia kama historia itajirudia tena.




