‘Tunataka kulipiza kisasi’-Bernardo Silva
BAADA ya kuitoa Bayern Munich katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kiungo wa Manchester City, Bernardo Silva ametabiri kuwa klabu yake itatinga fainali ya michuano hiyo.
Erling Haaland amefunga bao lake la 48 wakati City ikiwatoa mabingwa hao wa Bundesliga kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya sare ya bao 1-1 na kutinga nusu fainali dhidi ya Real Madrid.
Silva anaamini watalipiza kisasi dhidi ya Real, ambao waliwatoa katika muda wa nyongeza katika hatua hiyo hiyo msimu uliopita.
“Tutapambana kwa kweli. Siku zote tunapambana lakini tunahisi timu inajiamini sana kwa sasa. Nafikiri tutafuzu,” amesema Silva.
Kocha wa City Pep Guardiola amemwita Haaland ‘mashine ya ajabu’ baada ya mshambuliaji huyo kufanga bao la kuongoza na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufikisha mabao 35 barani ulaya.
Haaland ana umri wa miaka 22.