Shime:Tunataka Kombe la CECAFA nyumbani

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls), Bakari Shime amesema kikosi chake kipo tayari kwa changamoto ya michuano ya CECAFA itakayoanza kesho, akisisitiza dhamira yao ni kutetea heshima ya nyumbani kwa kubakisha taji hilo.
Shime amesema mashindano hayo hayatakuwa mepesi kutokana na kushirikisha timu saba zenye ushindani mkubwa, huku akizitaja Kenya na Uganda kuwa miongoni mwa timu zitakazotoa upinzani mkali.
“Kuna timu zenye ushindani mkubwa kama Kenya na Uganda ambao wako vizuri, hivyo tunafahamu mashindano yatakuwa magumu,” amesema Shime.
Kocha huyo alieleza kuwa kikosi chake kina faida ya kuwa na wachezaji wenye uzoefu wa mashindano ya kimataifa baada ya kushiriki mechi na mashindano mbalimbali katika nchi za Tunisia, Botswana na Afrika Kusini.
“Wachezaji wetu wana uzoefu wa kutosha, walipata nafasi ya kucheza Tunisia, Botswana na Afrika Kusini. Huo utaendelea kutusaidia kuongeza kiwango na kujiamini kwenye mashindano haya,” amesema.
Shime amesema benchi la ufundi limejipanga vizuri kuhakikisha timu inafanya vizuri na kufikia malengo waliyojiwekea katika mashindano hayo.
“Mashindano yanaanza kesho na ni matumaini yetu tutafanya vizuri. Deni tulilonalo pamoja na ugumu wa mashindano linatufanya tutamani kulibakisha kombe nyumbani. Kwa juhudi za wachezaji na mipango ya benchi la ufundi tunaamini tutafanya vizuri,” amesema.
Michuano hiyo inashirikisha timu za Tanzania, Zanzibar, Somalia, Djibout, Sudan Kusini, Uganda na Sudan ambapo watatumia viwanja vya KMC na Azam Complex.




