Serikali kupandisha kodi mirabaha taasisi za michezo

DODOMA:SERIKALI imependekeza kuongeza kiwango cha kodi ya zuio kwenye mrabaha kwa taasisi za michezo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoka asilimia tano hadi asilimia 10 kuanzia mwaka wa fedha 2026/27.
Hatua hiyo imetangazwa na Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar, wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27 Bungeni jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Lengo la hatua hii ni kuendana na kanuni za usawa za utozaji kodi kwa kuwa kiwango husika kinatozwa kwenye mrabaha kwa tasnia ya filamu.
“Pendekezo hili linalenga kuendana na kanuni za usawa za utozaji kodi kwa kuwa kiwango husika tayari kinatozwa kwenye mrabaha wa tasnia ya filamu,” amesema.
Iwapo mapendekezo hayo yatapitishwa na Bunge, Serikali inatarajia kuongeza mapato kwa kiasi cha shilingi bilioni 1.44 katika mwaka wa fedha ujao.




