Wasanii watakaoburudisha siku ya Mwananchi
DAR ES SALAAM: KLABU ya yanga imeweka wazi wasanii watakaoburudisha katika kilele cha wiki ya Mwananchi, Agosti 4, mwaka huu katika uwanja wa Benjamin Mkapa , jijini Dar es Salaam.
Wasanii hao ni Rajab Abdul ‘Harmonize’, Marioo na Christian Bella ambao watatoa burudani kabla ya Yanga kutambulisha wachezaji wao watakaowatumia msimu mpya wa mashindano.
Akizungumza na waandishi wa habari , Msemaji wa Yanga, Haji Manara amesema wasanii hao na wengine wataimba nyimbo maalum za kuisifia Yanga .
“Huu ni msimu wa kipekee, wasanii hawa ndio watakaotumbuiza lakini na utambulisho tutakaoufanya una hadhi kama ule uliowahi kufanyika Marekani. Jumapili tutakuwa na wasanii wakubwa na wenye vionjo tofauti tofauti ili kuhakikisha Wananchi wanapata burudani yenye hadhi ya klabu yetu”, amesema Manara.
Msemaji huyo amewatupia dongo wapinzani wao kuwa Yanga wanauza tiketi kwa kufuata utaratibu tofauti na wanavyofanya klabu nyingine, lakini siku ya jumapili, Agosti 4 mwaka huu itakata mzizi wa fitina baada ya mashabiki wao kujaza uwanja.
Yanga inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa katika siku ya kilele cha wiki ya Mwananchi dhidi ya Red Arrows ya Zambia ambao ni mabingwa wapya wa kombe la CECAFA.