Nyumbani

Yanga Veterani yalalamikia utata wa umri

DAR ES SALAAM: KOCHA wa Yanga Veterani, Ken Mkapa, ameibua mjadala kuhusu suala la umri katika mashindano ya maveterani akidai baadhi ya timu zinatumia wachezaji wanaoonekana kuwa na umri mdogo kuliko uliotarajiwa katika mashindano hayo.

Mkapa, ambaye ni beki wa zamani wa kushoto wa Yanga, amesema tofauti ya umri ilionekana wazi katika mechi yao ya hivi karibuni ambapo baadhi ya wapinzani walionysha kasi kubwa uwanjani ikilinganishwa na wachezaji wengi wa Yanga Veterani.

Amesema wengi wa wachezaji wake wana umri wa kati ya miaka 50 hadi 60, huku baadhi yao wakiwa na miaka 48 au 49, jambo linaloifanya timu hiyo kutegemea zaidi uzoefu na maarifa ya mchezo kuliko nguvu za mwili.

Kwa mujibu wa Mkapa, kanuni za mashindano zinaruhusu timu kutumia hadi wachezaji watano wenye umri wa miaka 35, lakini alisisitiza kuwa lengo la mashindano ya maveterani ni kutoa burudani kupitia nyota wa zamani waliowahi kung’ara katika soka.

“Ukiwaangalia baadhi ya wachezaji wa timu pinzani unaona wazi wana kasi kubwa sana. Hilo linaibua mjadala kuhusu umri katika mashindano haya,” amesema.

Hata hivyo, Mkapa amesema hataki kutumia suala hilo kama kisingizio cha matokeo baada ya timu yake kulazimishwa sare ya mabao 2-2 kabla ya kuondolewa kwa mikwaju ya penalty 4-2 dhidi ya Uhuru.

Amesema kuwa Yanga Veterani ilionesha ushindani mkubwa licha ya changamoto ya tofauti ya umri na kwamba matokeo hayo yanaonesha timu hiyo bado ina uwezo wa kushindana na yeyote.

Related Articles

Back to top button