Mwamuzi wa Somalia azuiwa kuingia Marekani, afukuzwa Kombe la Dunia

MAREKANI: NDOTO ya mwamuzi wa soka kutoka Somalia, Omar Abdulkadir Artan, ya kuchezesha mechi za Kombe la Dunia 2026 imefikia tamati ghafla baada ya kunyimwa ruhusa ya kuingia nchini Marekani, hatua iliyomfanya kuondolewa rasmi kwenye orodha ya waamuzi wa mashindano hayo.
Artan, ambaye alikuwa ameandika historia kwa kuwa Mwamuzi wa kwanza kutoka Somalia kuteuliwa na FIFA kwa ajili ya Kombe la Dunia, alizuiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami baada ya kuwasili akitokea Istanbul Uturuki mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mamlaka za uhamiaji za Marekani zilisema alifanyiwa ukaguzi wa kawaida kabla ya kutoruhusiwa kuingia nchini humo kutokana na kile kilichoelezwa kama hofu za kiusalama zilizoonekana katika mchakato wa uchunguzi.
Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, limethibitisha kuwa Artan hatoshiriki mafunzo wala kuchezesha mechi yoyote ya Kombe la Dunia kutokana na uamuzi huo wa mamlaka za Marekani.
Kabla ya tukio hilo, Artan alikuwa akitajwa kama mmoja wa waamuzi bora zaidi barani Afrika. Mwaka 2025 alitunukiwa tuzo ya mwamuzi bora wa kiume wa Afrika na Shirikisho la Soka Afrika, CAF, baada ya kuonesha kiwango cha juu katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Kuondolewa kwake kumewaacha wengi nchini Somalia katika hali ya masikitiko. Wadau wa soka nchini humo walikuwa wakiona uteuzi wake kama mafanikio makubwa kwa taifa ambalo limekuwa likijitahidi kujijenga upya katika michezo ya kimataifa kwa miaka mingi.
Katika taarifa yake, Artan amesema pamoja na changamoto hiyo ataendeleza taaluma yake ya uamuzi. Pia aliwashukuru FIFA na CAF kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kufikia hatua hiyo muhimu katika maisha yake ya soka.
Tukio hilo limezua mjadala mkubwa kimataifa, hasa kutokana na ukweli kwamba Artan alikuwa tayari amepata visa halali ya kusafiria Marekani kabla ya kuzuiwa kuingia nchini humo. Baadhi ya wachambuzi wamehusisha tukio hilo na sera kali za uhamiaji zinazowahusu raia wa baadhi ya mataifa, ikiwemo Somalia.
Kwa sasa, FIFA inatarajiwa kutangaza mwamuzi mwingine wa kuchukua nafasi ya Artan katika kikosi cha waamuzi wa Kombe la Dunia 2026.




