
LONDON: ALIYEKUWA nyota wa timu ya taifa ya England, James Milner, ametangaza kustaafu soka baada ya kucheza kwa miaka 24 katika Ligi Kuu ya England.
Kiungo huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali, ambaye sasa ana umri wa miaka 40, anaondoka uwanjani baada ya kumaliza mkataba wake na Brighton & Hove Albion, alikocheza kwa misimu mitatu iliyopita.
Milner ameandika historia kwa kucheza mechi nyingi zaidi katika Ligi Kuu ya England, rekodi aliyoiweka mwezi Februari mwaka huu.
Safari yake ya soka ilianza katika klabu ya Leeds United kabla ya kuendelea kung’ara katika klabu mbalimbali na kutwaa mataji matatu ya Ligi Kuu ya England; mawili akiwa na Manchester City na moja akiwa na Liverpool FC.
Pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Liverpool kilichoshinda taji la UEFA Champions League mwaka 2019.
Katika ujumbe wake wa kuaga kupitia mitandao ya kijamii, Milner amesema amebahatika kushuhudia nyakati nyingi za kipekee katika maisha yake ya soka, kuanzia mapambano ya kuokoa timu zisishuke daraja hadi kushinda mataji makubwa, kucheza mashindano ya Ulaya na kuiwakilisha England katika michuano miwili ya Ulaya na Kombe la Dunia mara mbili.
“Zaidi ya yote, nitayakumbuka milele mahusiano na urafiki nilioujenga kupitia mchezo huu,” amesema Milner.




