Arne Slot: Trent bado tunaye

BOSI wa Liverpool Arne Slot amesema beki wake wa kulia Trent Alexander-Arnold bado yupo sana Liverpool. Hii inakuja baada ya kuwepo kwa tetesi za nyota huyo mwenye kiwango bora msimu huu kutimkia kwa wababe wa La Liga Real Madrid mkataba wake utakapo malizika mwisho wa msimu huu.
Vyombo vya habari nchini England vimeripoti kuwa Real Madrid wameonesha nia ya kumsaini beki huyo lakini bado hawajatuma ofa rasmi kwa Liverpool na Slot anaamini beki huyo ataendelea kubaki Liverpool licha ya ‘kelele zenye lengo la kumpumbaza’
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo dhidi ya Manchester United Jumapili kwa kujiamini Slot amesema
“Naweza kukwambia kwamba atacheza Jumapili na tunaamini atacheza katika kiwango kile kile alichoonesha nusu msimu huu” alisema Slot.
“Nadhani kila mtu aliona jinsi alivyocheza nusu ya kwanza ya msimu alivyokuwa mzuri, ni kiasi gani moyo wake uko hapa, ni kiasi gani anataka kushinda makombe hapa. Ninamuona mazoezini, akijituma kila siku. Amejitolea kikamilifu kwetu na atacheza Jumapili na sina shaka atasalia Liverpool.”
Licha ya taarifa za TAA kumekuwa pia na uvumi juu ya mustakabali wa Mohamed Salah na Virgil van Dijk ambao pia wako ndani ya miezi sita ya mwisho ya mikataba yao Anfield.