West Ham kukabiliwa na ukata wa fedha

LONDON: KLABU ya West Ham United imeanza kukabiliwa na presha kubwa ya kifedha kufuatia uamuzi wa English Football League (EFL) kuanzisha sheria mpya za matumizi ya vikosi kuanzia msimu wa 2026-27.
Kwa mujibu wa sheria hizo mpya, klabu zitapaswa kutumia asilimia 85 tu ya mapato yao katika mishahara ya wachezaji pamoja na gharama nyingine za kikosi, jambo ambalo linaonekana kuwa changamoto kwa West Ham iwapo itashuka daraja kwenda Championship.
Ripoti ya mchambuzi wa fedha za soka Swiss Ramble imeeleza kuwa uwiano wa matumizi ya kikosi cha West Ham katika msimu wa 2024-25 ulikuwa asilimia 90 ya mapato ya klabu hiyo, kiwango kinachozidi kikomo kilichowekwa na EFL.
Katika taarifa za fedha za klabu hiyo, viongozi wa West Ham walikiri kuwa kushuka daraja kutakuwa na madhara makubwa kiuchumi na kunaweza kuilazimu klabu kuuza baadhi ya wachezaji wake ili kupunguza mzigo wa mishahara pamoja na kuongeza mapato kupitia ada za usajili.
“Hatari kubwa ya biashara ya klabu inaendelea kuwa kushuka daraja kwa timu ya wanaume kutokana na madhara makubwa ya kifedha yanayoweza kutokea,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Vyanzo vya ndani ya klabu hiyo vinaeleza kuwa mapato ya West Ham yanaweza kupungua kwa kati ya asilimia 50 hadi 60 endapo watashuka daraja msimu ujao.
Katika taarifa za fedha za hivi karibuni, West Ham ilitangaza mapato ya pauni milioni 227.6, yakishuka kutoka pauni milioni 269.7 mwaka uliopita, hali inayoongeza hofu ya athari za kifedha iwapo timu hiyo itapoteza nafasi yake katika Ligi Kuu England.




