Kwingineko

Pellegrini afurahia kurejea Ligi ya Mabingwa

SEVILLA: KOCHA wa Real Betis, Manuel Pellegrini amesema ana furaha kubwa baada ya timu hiyo kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20.

Betis ilihakikisha nafasi hiyo baada ya kuifunga Elche mabao 2-1 katika mchezo wa LaLiga, ushindi uliowafanya kumaliza ndani ya nafasi tano za juu kwenye msimamo wa ligi.

Pellegrini amesema kufuzu huko ni matokeo ya malengo waliyojiwekea tangu mwanzo wa msimu pamoja na kazi kubwa iliyofanywa na wachezaji wake.

“Si jambo rahisi kucheza michuano ya Ulaya kwa miaka sita mfululizo, lakini kufuzu Ligi ya Mabingwa kabla ya msimu kuisha ni mafanikio makubwa sana,” amesema Pellegrini.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 72 amesema moja ya siri ya mafanikio yao ni uwezo wa timu kurejea kwa nguvu kila ilipopata matokeo mabaya.

“Ubora mkubwa wa timu hii ni namna ilivyokuwa ikiinuka kila baada ya kuanguka. Mashabiki wetu walistahili furaha hii kubwa,” amesema.

Pellegrini amesema tangu mchezo wa kwanza wa msimu dhidi ya Elche waliweka wazi ndoto yao ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Baada ya mazungumzo ya kwanza ya msimu tuliandika kwa rangi ya kijani kuwa safari ya kuelekea Ligi ya Mabingwa inaanza sasa,” amesema.

Real Betis imekuwa ikipewa sifa kwa mwendelezo mzuri wa ushindani katika michuano ya Ulaya tangu mwaka 2021, huku msimu uliopita ikifika fainali ya UEFA Conference League.

Related Articles

Back to top button