Yanga, Dodoma Jiji lazima kieleweke

SINGIDA: KOCHA wa muda wa Yanga, AbdiHamid Moallin, amesema kikosi chake kiko tayari kupambana na Dodoma Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Airtel mkoani Singida.
Moallin amesema licha ya ratiba kuwa ngumu kutokana na muda mfupi kati ya mechi moja na nyingine, benchi la ufundi limejikita zaidi katika kuhakikisha wachezaji wanapata mapumziko ya kutosha ili wawe katika hali nzuri ya ushindani.
“Tumefanya maandalizi mazuri. Muda kati ya mchezo uliopita na huu ni mfupi, hivyo tulihakikisha wachezaji wanapata muda wa kupumzika na kuwa tayari kwa mchezo wa kesho,” amesema Moallin.
Amesema anatarajia mchezo mgumu dhidi ya Dodoma Jiji kutokana na ubora wa wapinzani wao, lakini anaamini Yanga ipo tayari kuondoka na pointi tatu muhimu.
“Itakuwa mechi ya ushindani mkubwa dhidi ya timu nzuri ya Dodoma Jiji. Tunajua kazi iliyotuleta hapa ni kupata ushindi,” amesema.
Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya kucheza michezo 22, ikishinda mechi 16 na kutoka sare sita huku ikiwa haijapoteza mchezo wowote msimu huu.
Mabingwa hao watetezi pia wamefunga mabao 50 na kuruhusu mabao matano pekee, rekodi inayodhihirisha uimara wao katika mbio za ubingwa.
Moallin amesema kila mchezo uliobaki ni muhimu kwao kutokana na presha kutoka kwa wapinzani wao wa karibu Simba SC ambao wanaendelea kuwafukuzia kwenye msimamo wa ligi.
Kocha huyo pia ametoa taarifa ya hali ya kikosi akieleza kuwa wachezaji wengi wako tayari kwa mchezo huo isipokuwa Mohammed Hussein ambaye bado anaendelea kurejea taratibu baada ya kuumia.
Aidha, kurejea kwa kiungo Mudathir baada ya kumaliza adhabu ya kusimamishwa kutakuwa nyongeza muhimu kwa kikosi hicho katika kipindi hiki cha mwisho wa msimu.
Kwa upande wa Dodoma Jiji FC, Kocha Amani Josiah amesema benchi lake la ufundi pamoja na wachezaji wako tayari kwa mchezo huo mkubwa dhidi ya Yanga huku akieleza kuwa hawana presha yoyote licha ya kukutana na vinara wa ligi.
“Benchi la ufundi liko tayari. Tunajua tunacheza na timu ambayo inapigania ubingwa hivyo ni mechi ya ushindani mkubwa, lakini sisi hatuna presha yoyote. Tutapambana na kuonesha kile tunachokimiliki uwanjani,” amesema Amani Josiah.
Takwimu zinaonesha Yanga imeshinda michezo mitano iliyopita dhidi ya Dodoma Jiji, ikiwemo ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza msimu huu.




