Ligi Kuu

Moallin: Tunazitaka pointi tatu kwa Coastal

DAR ES SALAAM:KAIMU Kocha Mkuu wa Yanga, Abdihamid Moallin amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa kesho Mei 9,2026 dhidi ya Coastal Union utakaochezwa katika Uwanja wa KMC huku akisisitiza kuwa lengo kubwa ni kupata pointi tatu.

Moallin amesema wachezaji wako kwenye hali nzuri kiakili na kimwili kuelekea mchezo huo muhimu, akieleza kuwa kila mmoja anatambua umuhimu wa mechi hiyo katika mbio za timu yao.

“Wachezaji wako kwenye morali nzuri na tunajua huu ni mchezo muhimu sana kwetu. Tunaamini tutakwenda uwanjani kutoa kiwango bora na kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema Moallin.

Amesema kwa sasa benchi la ufundi halifikirii malengo ya muda mrefu bali limeweka nguvu zote katika mchezo huo dhidi ya Coastal Union ili kuongeza pointi tatu nyingine kwenye msimamo wa ligi.

Moallin pia amesisitiza kuwa Yanga kama mabingwa watetezi wa ligi kwa misimu minne mfululizo wana wajibu mkubwa wa kuonesha kiwango bora uwanjani sambamba na kucheza soka la kuvutia mashabiki wao.

“Mashabiki wetu wanapenda soka la kushambulia na la kuvutia. Kikosi chetu kimejengwa kwa ajili ya kucheza mpira wa kushambulia, kushinikiza juu na kucheza kwa kasi,” amesema.

Kocha huyo ameongeza kuwa malengo yao ni kuutawala mchezo kwa dakika zote 90 badala ya vipindi vifupi vya mchezo, huku akiahidi timu kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha inaondoka na ushindi mbele ya Coastal Union.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button