Nyumbani

Magori: Simba bado haijafikia kiwango tunachotaka

ZANZIBAR:MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, amesema licha ya timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano, bado hajaona kiwango kinachoridhisha kulingana na malengo ya klabu hiyo.

Akizungumzia ushindi huo, Magori amesema mchezo ulikuwa mgumu kwa kuwa ulidumu kwa dakika 120 za “jasho na damu”, hali iliyowachosha wachezaji kuelekea mechi nyingine muhimu inayofuata ndani ya siku chache.

“Mechi ilikuwa ngumu sana, dakika 120 za jasho na damu. Bado tuna siku mbili au tatu tunaenda kucheza mechi nyingine ngumu sana, hivyo wachezaji wanatakiwa kupona haraka kujiandaa na mechi ya Jumapili,” amesema.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa bado hajaridhishwa na kiwango kilichooneshwa na timu hiyo, akibainisha kuwa Simba hailengi zaidi mafanikio ya ndani bali kimataifa.

“Bado sijaridhishwa na kile nilichokiona. Timu yetu inapaswa kucheza zaidi ya hapa tulipofikia kwa sababu tunaunda timu si kwa ajili ya Ligi ya Tanzania tu, bali kwa ajili ya kushindana Afrika. Hii timu bado inajengwa,” amesema.

Magori pia alimpongeza Rais wa Klabu hiyo, Mohamed Dewji, kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya timu, hususan kwenye usajili na uendeshaji wa klabu.

“Namshukuru sana Mo Dewji kwa kujitolea kwake, amekuwa akitoa fedha za usajili na kuisapoti timu. Wanasimba wanapaswa kuendelea kumuunga mkono,” amesema.

Related Articles

Back to top button