Serikali kujenga shule 56 za kuinua vipaji vya michezo nchini

DAR ES SALAAM: SERIKALI ina mpango wa kujenga shule 56 maalumu za kukuza vipaji vya watoto kuanzia umri mdogo, ambapo ujenzi utaanza kwa shule saba katika kila halmashauri nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Leo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake katika Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa, Waziri Habari wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema shule hizo zitalenga kuwaandaa watoto wenye vipaji mbalimbali hususan michezo ili kuviendeleza mapema.
Makonda amesema uwepo wa shule zinazozingatia vipaji utaisaidia nchi kupata wanamichezo bora, huku klabu zikipata urahisi wa kusajili wachezaji waliokwisha andaliwa kitaaluma na kimichezo.
“Tukiwa na shule za vipaji, hata klabu zinapohitaji wachezaji zitawachukua moja kwa moja kutoka shuleni ambako wanapata muda wa mazoezi na kujiimarisha,” amesema Makonda.
Aidha, amewahimiza wawekezaji wa sekta binafsi kuwekeza kwenye michezo, akisema Wizara iko wazi kwa yeyote mwenye nia ya kujenga au kuanzisha shule na miundombinu ya michezo.
Katika hatua nyingine, Makonda amesema Serikali itaandaa walimu, makocha na wakufunzi wa kutosha pamoja na mitaala bora kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na TAMISEMI ili kusaidia kukuza vipaji vya watoto.
Amefafanua kuwa asilimia 60 ya mafunzo yatakuwa ya nadharia huku asilimia 40 yakitolewa kwa vitendo, lengo likiwa ni kuzalisha wachezaji wengi watakaouzwa nje ya nchi.
Makonda ameongeza kuwa michezo, nyimbo, vyakula na mavazi ya Kitanzania vina nafasi kubwa ya kulitangaza Taifa kimataifa, huku michezo ikichangia kuongezeka kwa idadi ya wageni wanaotembelea nchini.
Kuhusu miundombinu, amesema Uwanja wa Arusha unaongoza kwa ubora ikilinganishwa na viwanja vingine, huku Uwanja wa Benjamin Mkapa ukiendelea kufanyiwa maboresho ya mfumo wa maji na maeneo ya VIP ili kuendana na hadhi ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Amesema pia ujenzi wa Uwanja wa Dodoma unaendelea na Uwanja wa Uhuru utakarabatiwa ili kuweza kutumika kwa michezo mbalimbali.
Makonda ameeleza kuwa Serikali iko katika mchakato wa kubadilisha sheria na kanuni za elimu ili kutoa nafasi zaidi kwa vijana wenye vipaji vinavyochipukia.




